Description
SHERIA HAIZUNGUKIKI
Kifungu cha sheria kikishaelekeza kitu kwa uwazi, ni hatari kujaribu kukizunguka hicho kifungu. Mfano mzuri ni kilichotokea kwenye hii kesi. Kulikuwa na wahusika watatu ambao, kwa lugha nyepesi tutawaita NEN, MMW na MRS. MM. Mhusika wa kwanza, NEN, alikuwa mke wa MMW wakati MRS. MM ni mama mzazi wa MMW. Kesi ilikuwa inahusu mambo mbalimbali lakini hapa tutaangalia jambo moja ambalo lilikuwa umiliki wa ardhi na nyumba iliyoko kwenye ardhi hiyo.
NEN alidai kwamba ardhi inayogombaniwa ni mali ya ndoa. Kulingana na Ushahidi wake, mumewe ndiye aliyenunua hiyo ardhi lakini akamwandika mama yake kama mmiliki kwa kuwa wakati ununuzi huo ukifanyika mume hakuwa raia wa Tanzania na hivyo hakuwa na haki ya kumiliki ardhi (uk. 20). Kama kweli hicho ndicho kilichotokea, ni wazi kwamba NEN na MMW walikuwa wanajaribu kuizunguka sheria ambapo MMW alitaka kupata haki ya kumiliki ardhi kwa mlango wa nyuma wakati sheria imeshamnyima haki hiyo.
Katika kuamua mgogoro huo, Mahakama ilikataa madai ya NEN kwa sababu hakukuwa na ushahidi. Ardhi ilionekana ni mali ya MRS. MM kwa kuwa ndiye aliyekuwa amesajiliwa kwenye hati.
Pamoja na hayo, hata kama NEN angekuwa na ushahidi wa kutosha wa kimaandishi unaoonesha kwamba kweli MMW ndiye aliyenunua ardhi hiyo, bado shida ingekuwepo kwa kuwa MMW hakuwa raia wa Tanzania wakati ardhi hiyo inanunuliwa na hivyo hakuwa na haki ya kumiliki ardhi hiyo. Mauzo kati ya MMW na mmiliki wa awali yangeonekana ni batili kwa kuwa sheria ya ardhi inazuia mtu asiye raia wa Tanzania kumiliki ardhi Tanzania.
Ni hatari kubwa kujaribu kuizunguka sheria kwa nia ya kupata haki ambayo sheria yenyewe imeshatamka wazi kwamba haki hiyo haipo. Mtu akifanya hivyo inakuwa ni sawa na kukalia kuti kavu ambalo saa yoyote linaweza kukatika na kumletea madhara makubwa.
Ni wazi pia kwamba kitendo cha mtu kununua ardhi au mali nyingine na kuandika jina la mtu mwingine akidhani hiyo ardhi itakuwa mali yake ni makosa makubwa. Mmiliki halali atakayelindwa na sheria ni yule anayesomeka kwenye makaratasi bila kujali kama kweli yeye ndiye aliyetoa hela ya manunuzi au la. Sheria inamtambua mmiliki anayesomeka kwenye makaratasi tu.